NA YASSIR MKUBWA - ZANZIBAR TODAY
JUMLA ya mama 100 na watoto 100 wamepatiwa bima kubwa ya bure ya mwaka mzima na kampuni ya Teknologia na mawasiliano Vodadom Tanzania.Kina mama hao ni wale waliojifungua watoto wao kunazia Novemba 9 mwaka huu katika hospitali ya Rufaa Mnaznimmoja kupatiwa zawadi hiyo ya upendo.
Akizungumza katika hafla ya kukabidhi bima hizo Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano Vodacom Tanzania, Anet Kanora, alisema hatua hiyo ni muendelezo wa kampuni hiyo kutoa zawadi kwa wateja wake ikiwa ni njia ya kuwashukuru lakini kwa mwaka huu wameona ipo haja ya kuifikia jamii pana ya watanzania.
Alisema afya ya mama na mtoto ni muhimu kwa kampuni hiyo hivyo wameona ipo haja ya kumpatia bima kubwa mama pamoja na mtoto wake itakayomuwezesha mama na mtoto wake kupata matibabu.
Aidha alisema kwa Tanzania nzima bima hiyo itanufaisha watoto 1000 na mama 1000 lakini kwa Zanzibar kinamama 100 na watoto 100 watanufaika na bima hiyo ya afya.
Alisema bima hizo zitatumika katika hospitali mbalimbali za Zanzibar ikiwemo Ampola Global, Tawakal, Alrahma na hospitali ya Rufaa Mnazimmoja kwa Zanzibar na hospitali ya Muimbili na nyengine za Tanzania bara.
Mkuu Anet alibainisha kuwa bima hiyo itakuwa haina upendeleo kwani ni lazima watoto wote watakaozaliwa katika kipindi hichi basi wote watanufaika na bima hiyo kuona wanatibiwa magonjwa mbalimbali ikiwemo ya kulazwa ama kutibiwa na kuondoka.
Alibainisha kuwa anaamini bima hiyo itakwenda kuwasaidia wazazi na watoto wao kwani mwaka wa kwanza wa mtoto ni muhimu sana katika upimaji na upatikanaji wa afya bora katika makuzi ya mtoto.
Akizungumzia kuhusu kampeni ya ‘Sambaza Shangwe, Gusa Maisha’ Meneja Mauzo Vodacom Zanzibar, Fadhili Linga, alisema kampeni hiyo ina sehemu mbili, kwanza kuwazawadia wateja kwa zawadi mbalimbali na pili kujikita katika shughuli za kijamii.
Linga alisema sekta ya afya ni eneo muhimu na kampuni hiyo imeona iendeleze jitihada za kuunga mkono serikali kupitia miradi mbalimbali.
Aliahidi kuwa watanendeleza ushirikiano huo ili kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora za matibabu ya afya kwa Watanzania wote zinapatikana bila ya usumbufu.
Alisema mbali na kutoa bima pia Vodacom imekuwa ikiwazawadia zawadi kama vile bodaboda, TV, simu za mkononi, router za 4G na 5G na pesa taslimu kuanzia shilingi 500,000 mpaka milioni 10,000,000.
Khadija Salum Said ni Mkuu wa Wodi ya Wazazi hospitali ya Rufaa Mmnazimmoja, aliipongeza kampuni hiyo kwa ubunifu wa kampeni hiyo ambayo inawajali kinamama wanaoleta viumbe wapya duniani.
Alisema kupatiwa bima hizo itasaidia kwa kiasi kikubwa kupatikana kwa huduma ya uhakika ya afya katika hatua ya awali ya watoto wachanga na akina mama waliotoka kujifungua na kupunguza vifo vya mama na watoto wachanga.
Kwa kupatia bima ya afya ya bure, tena ile kubwa kwa mwaka mzima, akina mama hawa na watoto wao hawatokuwa na shaka pindi watakapokumbwa na changamoto za kiafya, ujio wenu huu umetusaidia sana kupunguza matatizo ambayo yatatokea baada ya mama kujifungua na hata kupunguza vifo vya watoto wachanga,”alisema.
Hivyo, aliiomba kampuni hiyo kuendelea kushirikiana pamoja katika mapambano ya kupunguza vifo vya mama na mtoto kwa kusaidia bima hiyo kwa wazazi wa Tanzania nzima kwani utoaji wa bima hiyo ni njia moja ya kupunguza vifo hivyo.
Wakizungumza kwa niaba ya wazazi wenzao waliopatiwa bima hizo Maryam Yohana Daniel na Badria Mohammed Khamis aliejifungua watoto mapacha walipongeza Vodacom kwa kuwapatia bima hizo ambazo zitawasaidia kupata matibabu wao na watoto wao na huduma nyengine za kiafya.
Hivyo waliiomba jamii kujiunga na kampuni ya Vodacom ili iweze kusaidia kundi kubwa zaidi katika jamii ya watanzania.
VodaBima itawawezesha akina mama na watoto wao kupata huduma za afya ni sehemu ya kampeni inayoendelea ya kampuni hiyo nchini kote ijulikanayo kama ‘Sambaza Shangwe, Gusa Maisha’.