Sunday, 13 October 2024

ZMA YARIDHIA ONGEZEKO LA BEI YA NAULI ZA BOTI WASAFIRI WALALAMIKIA HALI


Na  Yassir Mkubwa El Bahsaany

 MAMLAKA ya Usafiri Baharini imesema serikali imeridhia kampuni za uwekezaji nchini zinazotoa huduma za usafiri wa Baharini kuongezeka bei za nauli za usafiri kutoka Dar es Salam na Ulnguja  kwa daraja la chini kutoka shilingi 30000 hadi 35000 ambazo zilianza kitumika rasmi Oktoba 7 mwaka huu.

Akizungumza na vyombo vya habari katika ofisi za mamlaka hiyo Bandarini  Mkirugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo Mtumwa Said, alisema kiridhia kwa ombi hilo kunatokana na hoja zilizowasiahwa na kampuni hizo juu ya ongezeko la nauli katika boti.

Akizitaja hoja zilizowasilishwa na kampuni hizo za usafirishaji alisema ni kuongezeka kwa Bei za gharama za mafuta ambapo kampuni zilieleza kuwa Bei ya nauli kwa tiketi ya shilingi 30,000 kwa daraja la chini ilitangazwa mnamo mwaka 2022 ambapo kwa wakati huyo bei  ya mafuta ulikuwa ni shilingi 2500 ikilinganishwa na mwaka huu ambapo Bei ya mafuta ni shilingi 3020 kwa lita.

Alisema ongezeko hilo limepelekea gharama za uendeshaji kuongezeka kwa asilimia 21 na Bei ya tiketi imeendelea kubaki ile ile.

Mkirugenzi Mtumwa alisema hoja nyengine ni kupanda kwa Bei ya fedha ya dola za kimarekani dhidi ya shilingi za kitanzania kwani kikawaida kampuni hizo zimekuwa zikilipa Kodi, kununua vifaa pamoja na kufanya matengenezo ya vyombo vyao kwa kutumia dola badala ya shilingi za kitanzania.

Alifahamisha kuwa mwaka 2022 dola ulikuwa sawa na shilingi za kitanzania 2,330 ambapo mwaka huu dola 1 ni sawa na shilingi 2,850 katika soko la kawaida ambayo hufanya ongezeko la asilimia 22 ya uendeshaji huku kampuni zimekuwa zikilipa Kodi TRA kwa dola badala ya shilingi ya kitanzania jambo linalopelekea pia kuongezeka kwa gharama za uendeshaji.

Hata hivyo sababu nyengine alisema ni gharama za matengenezo na utawala ambapo kampuni zililalamika kuongezeka kwa gharama za utawala na matengenezo ya vyombo kwa kipindi hichi ambapo dola imepanda ikilinganishwa na Bei ya abiria Kama ilivyo kwa kipindi Cha miaka miwili iliyopita.

Alisema serikali ilizijadili hoja hizo pamoja na kizofanyia uchambuzi taarifa zote za kifedha za uendeshaji za kampuni hizo na kubaini kwa kiasi haziendani na Bei halisi iliyokiwa ikitozwa hapo awali ya shilingi 30,000.

"Bei iliyowasilishwa awali na iliyopatikana ilikiwa ni zaidi ya shilingi 35000 iliyokibaliwa hivi sasa, serikali kwa kuzingatia hali za maisha ya wananchi wake hasa wa daraja la chini katika mazungumzo yaliyofanyika tuliwaomba sana wawekezaji/ kampuni hizi kukubali ombi la serikali kufikia shilingi 35000 kwa daraja la chini na kampuni zilitukubalia," alisema.

Hivyo aliwakumbusha wadau wote wa usafirishaji Baharini kuzingatia Bei iliyoidhinishwa na serikali na kufanya tofauti ni kwenda kinyume na Sheria na kampuni za usafiri Baharini na hatua kali za kisheria  zitachukuliwa kwa watakaobainika.

Sambamba na hayo aliwasisitiza wananchi kununua tiketi katika ofisi rasmi za kampuni za meli au boti na kuacha kununua tiketi za kusafiria kwa walanguzi na kupelekea kuuziwa kwa Bei za juu.

Mbali na hayo aliwakumbusha wamiliki wa vyombo vya usafiri kuzingatia Sheria, kanuni na miongozo yote inayosimamia usalama katika usafiri wa Baharini ikiweno kupakia abiria kwa mujibu wa uwezo wa chombo kama ilivyoidhinishwa na mamlaka 

Aliahidi kuwa mamlaka itaendelea kusimamia jukumu lake kwani ndio mamlaka yenye dhamana ya Usafiri Baharini Zanzibar.

Nao wananchi wanaotumia huduma hzo za usafiri Said Ali Abdalla, Juma Daud Ali na Salma Juma khalfan walisema  wamesikitishwa sana na  ongezeko hilo la bei kwani wananchi wengi hali zao ni duni na wanafanya shughuli zao za kujitafitia kipato.

Walisema ni vyema serikali kuwaangalia kushushwa kwa bei hiyo kwani tiketi  zipandishwa mara kwa mara na wengi wanaosafiri kutoka Unguja kwenda Dar es Salam wanakwenda kwa ajili ya kufanya biashara kujitafutia kipato Cha kuendesha familia zao.


Mwisho




Wednesday, 2 October 2024

 TUME Huru ya Taifa ya Uchaguzi katika kuhakikisha kwamba inaenda sambamba na mabadiliko ya teknolojia ikiwa ni pamoja na kurahisisha zoezi la uboreshaji wa daftari la wapiga kura, imeboresha mfumo wa uandikishaji ambao kwa mara ya kwanza utamuwezesha mpiga kura aliyepo kwenye daftari kuazisha mchakato wa kuboresha taarifa zake kwa kutumia simu ya kiganjani au komputa.

Hayo yalisemwa na Mjumbe wa Tume hiyo ambae pia ni Jaji wa Mahakama kuu Asina Abdallah Omar wakari akifunguwa mkutano wa tume hiyo kwa wadau wa uchaguzi katika ukumbi wa Sheikh Idrisa Abdulwakil Kikwajuni Mjini Zanzibar.

Jaji Asina alisema wanaotumia simu za viswaswadu nao hawakuachwa nyuma wanaweza kutumia huduma hiyo na kupata maelekezo pamoja na taarifa zao.

Alisema mzunguko wa sita wa uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura unatarajiwa kuanza Oktoba saba mwaka huu na kukamilika Oktoba 13 mwaka huu kwa visiwa vya Unguja na Pemba.

“Uboreshaji huu kama ilivyokuwa uboreshaji wa mwaka 2015 na 2020 utahusisha matumizi ya teknolojia ya biometric votes registration (BVR) ambapo mfumo huu hutumika katika kumtambua mtu na kumtofautisha na mwingine kwa kuwa unahusisha uchukuaji wa alama za vidole vya mikono, picha na saini na kuhifadhiwa kwenye kanzidata ya wapiga kura”alisema Jjai Asina.

Alisema uboreshaji huo ni tofauti na wa mwaka 2015/2020 ambapo ubereshaji wa mwaka huu utatumia teknolojia ya BVR Kits zilizoboreshwa kwa kuwekewa program endeshi ya kisasa zaidi na pia BVR zitakazotumika zimepunguwa uzito ambapo zitakuwa rahisi kubebeka na kufanya zoezi la ubereshaji wa daftari kuwa rahisi haswa kwenye maeneo ya vijijini na watendaji hulazimika kubeba vifaa kwa umabali mrefu.

Aidha alisema kujiandikisha kuwa mpiga kura zaidi ya mara moja ni kosa la kisheria kwa kuzingatia masharti ya kifungu cha 114(1) cha sheria ya uchaguzi wa Rais, wabunge na madiwani namba moja ya mwaka 2024.

Alisema kifungo hicho kinaeleza kuwa mtu yoyote atakayeomba kuandikishwa zaidi ya mara moja atakuwa ametenda kosa la kisheria na akituwa hatiani adhabu yake ni faini isiyopunguwa kiasi cha shilingi 10,0000 na isiyozidi shilingi 30,0000 au kutumikia kifungo kwa kipindi kisichopunguwa miezi sita na kisichozidi miaka miwili gerezani au vyote kwa pamoja kulipa faini na kifungo gerezani.

“Natumia fursa hii kuwaasa wananchi kujiepusha na kosa la kujiandikisha zaidi ya mara moja na niwaombe wadau mkawaelimishe wananchi kwamba wakajiandikishe mara moja na kwenye kituo kimoja ili kuepuka uvunjaji wa sheria”alisema mjumbe huyo wa Tume.

Hata hivyo alisema Tume imeweka utaratibu kwa watu wenyeulemavu, wazee, wagonjwa, wajawazito na akinamama wenye watoto wachanga watakaokwenda nao vituoni kupewa fursa ya kuhudumiwa bila kupanga foleni lakini zoezi hilo la ubereshaji la daftari la wapiga kura halitawahusu wapiga kura wenye kazi za tume, hawajahama kutoka eneo moja la uchaguzi kwenda eneo jingine au kuboresha taarifa zao.

Aliwataka wadau wa uchaguzi kuwafahamisha wananchi wenye sifa kujitokeza kwa wingi kujiandikisha au koboresha taarifa zao vituoni kwa kuwa utaratibu mzuri wa kuwahudumia umewekwa.

Akiwasilisha mada ya uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura, mwakilishi wa Mkurugenzi wa uchaguzi wa Tume hiyo huru ya Taifa Kailima Ramadhani, alisema zoezi la uboreshaji nchi nzima linatarajiwa kukamilika Machi mwakani ambapo litahusisha mambo mbalimbali ikiwemo kutoa kadi mpya kwa wapigak ura waliopoteza kadi au kadi kuharibika,kuondoa wapiga kura waliokosa sifa kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kuukana uraia wa Tanzania na kifo.

Aliwataja ambao hawana sifa ya kuandikishwa katika daftari la wapiga kura ni mtu aliopo chini ya kiapo cha utii wa nchi nyingine tofauti na Tanzania,amewekwa kizuwizini kama mhalifu mwenye ugonjwa wa hana akili, amewekwa kizuwizini kwa ridhaa ya Rais, ametiwa hatiyani kwa kosa ambalo adhabu yake ni kifo na anaetumikia kifungo kwa kosa ambalo adhabu yake inazidi miezi sita iliyotolewa na Mahakama.

Aidha alisema wapiga kura 5,586,433 wapya wanatarajiwa kuandikishwa sawa na asilimia 18.7 ya wapiga kura 29,754,699 waliopo kwenye daftari baada ya uboreshaji uliofanyika mwaka 2019/2020 na wapiga kura 4,369,531 inatarajiwa watabresha taarifa zao.

“Wapiga kura 594,494 inatarajiwa wataondolewa kwenye daftari hivyo baada ya uboreshaji, inatarajiwa kuwa daftari litakuwa na jumla wa wapiga kura 34,746,638”alisema Mkurugenzi huyo.

Wakizungumza katika mkutano huo wadau wa uchaguzi walioshiriki mkutano huo, walisema kuwa zoezi hilo la uboreshaji ni muhimu ambapo wananchi watapata haki yao ya kuandikishwa na kupiga kura katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.