Na Seif Mbarouk - Malindi
Wavuvi mbali mbali wametakiwa kuunga mkono shamrashamra za wiki ya uvuvi katika ukataji wa leseni za uvuvi ili kuachana na uvuvi haramu unaoendelea kufanyika siku hadi siku.
Amesema hayo Meneja wa Diko na Soko la Samaki la Malindi Nd. Mohd Idarus Mohd wakati wa ufanyaji wa usafi wa soko la samaki pamoja na upimaji wa afya kwa wananchi huko Malindi Mkoa wa Mjini Unguja.
Meneja huyo amesema miongoni mwa shamrashamra za wiki ya mvuvi ni kuwahamasisha wavuvi kufuata sharia za uvuvi ikiwemo ukataji wa leseni kwa ajili ya kuimarisha shughuli za uchumi wa buluu nchini.
Sambamba na hayo amesema lengo la kuadhimisha siku ya Mvuvi Duniani nu kujadili mambo mbali mbali yanayohusiana na uvuvi ili kutambua umuhimu wa sekta ya uvuvi pamoja na kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta hiyo.
Kwa upande wake Mratibu wa Kifua Kikuu Zanzibar Dkt. Rahma Omar kutoka Shirika la Amred Tanzania amesema lengo la kuendesha shughuli za afya katika Soko la Malindi ni kuwasogezea huduma kwa karibu ili kuwakinga na hatari ya kupata ugonjwa wa kifua kikuu.
Vilevile amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imegharamia huduma za afya kwa wananchi hivyo wananchi mbalimbali wanapaswa kujitokeza kwa wingi kupata huduma mbalimbali kama upimaji wa shindikizo la damu ,homa ya ini ,kisukari na mengineo.
Kwa upande wao Washiriki wa zoezi hilo wamesema wameishukuru Serikali kwa kuadhimisha siku ya Mvuvi Duniani kwa kuwaletea huduma ya afya bure na kutoa wito kwa wavuvi wa diko la Malindi kuja kushiriki zoezi hili ili kuwa na uhakika wa afya zao.
MWISHO.
No comments:
Post a Comment