DK. MWINYI AKAMILISHA ZIARA YAKE PEMBA
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Al hajj. Dk. Hussein Ali Mwinyi amehimiza jamii kuweka mkazo zaidi kwenye malezi ya watoto na vijana ili kukuza taifa lenye maadili, nidhamu na kizazi chema chenye kumjua Mwenyezi Mungu.
Al hajj Dk. Mwinyi aliyasema hayo kwenye kilele cha maadhimisho ya Mwaka mpaya wa Kiislam Zanzibar, 1445 Hijria, masjid Munawwara, Mfikiwa Mkoa wa Kusini, Pemba.
Alisema, ni wajibu wa wazazi na walezi kuwasimamia vyema watoto wao na kuwapa elimu ya dini na dunia ili kuwaepusha na vitendo vya uvunjivu wa amani, tabia mbaya na vitendo vya udhalilishaji.
Akizungumzia historia ya tarehe ya Kiislaam, Al hajj Dk. Mwinyi alieleza ilianza mara baada ya Mtume SAW kuhama Makka na kuhamia Madina ambako utulivu na Amani ulipatikana na kuwa chanzo cha kuenea uislam dunia nzima.
Alisema lengo la kuadhimishwa mwaka Mpya wa Kiislam 1445 H ni kuendelea kusisitiza na kuhimiza amani, ushirikiano na upendo kwenye jamii Katika kutekeleza mambo ya heri.
Aidha, aliendelea kuhimiza Umoja na mshikamano kwenye jamii ili nchi izidi kupata neema na baraka kutoka kwa Mola.
Akizungumza kwenye hafla hiyo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Haroon Ali Suleiman, alipongeza ushirikiano uliopo baina viongozi wa Mkoa wa Kusini na Kaskazini Pemba na viongozi wa Chama, katika kutela Maendeleo ya kisiwa hicho.
Akiwasilisha mada nidhamu ya kodi kwenye kongamano la mwaka mpya wa kiislaam 1445, Sheikh Said Ahmad aliwataka watumishi wa Umma kuutumia vyema muda wa Serikali wanapokua kwenye majukumu yao ili kukwepa kuchuma mali za dhulma zinazotokana na utumishi waa hasa kwenye ibada zao.
Pia alihimiza umuhimu wa kulipa Kodi kwa serikali kwa mujibu wa sheria za Kiislam.
Naye Sheikh Izud Alaw wa Mombasa Kenya, aliwahimiza waumini wa Kiislam juu ya umuhimu wa kuzingatia vyema tarehe za kiislam kwenye mfumo wa maisha yao.
Pia alieza miezi ya Kiislaam inabeba mfumo mzima wa maisha ya binaadam.
Vile vile, aliwataka waumini wa dini ya Kiislaam kutofungamana na kufuatilia masuala na muandamo wa mwenzi na hitilafu za Arafa pekee pia waangalie mambo mengine muhimu ikiwemo suala la eda kwa mwanamke alieacha ama kufiliwa na mumewe kwa tarehe zinapoanza hadi kumalizika kwake.
Akiwasilisha taarifa ya maadhimisho ya mwaka mpya wa Kiislam 1445, Katibu Mtendaji wa Ofisi ya Mufti , Sheikh Khalid Mfaume, alisema lengo la maadhimisho hayo ni kuitangaza tarehe ya kiislam na kuendeleza historia ya dini walioiacha maulamaa na kuahidi ofisi ya Mufti inajukimu ya kuendelea kuitangaza na kuishajisha kwa jamii.
Alisema maadhimisho ya mwaka mpya wa Kiislam yalifanikishwa kwa matukio mbalimbali ikiwemo kutoa huduma za macho kwenye hospitali ya kivunge, Mkoa wa Kaskazini Unguja, kusomwa dua ya kuliombea Taifa, kufanikishwa kwa kongamano kuwa la wanawake wa Kiislam lililohudhuriwa na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Hajjat Dk. Samia Suluhu Hassan, maonesho ya kiislam ya biashara yaliyowashirikisha wafanyabiasha wadogo na wajasiriamali, matembezi ya Zafa, kisiwani Pemba yaliolenga kuboresha afya pamoja na matembezi ya hiari yatafanyika Unguja.
MWISHO.
No comments:
Post a Comment